Wanaume rahisi kupata HIV kwa wajawazito

Watafiti wamesema, wanaume wana hatari ya kuambukizwa virusi vya ukimwi mara mbili iwapo mwenzao ni mjamzito.

Image caption Chembechembe ya HIV

Utafiti wa zaidi ya wapenzi 3,000 barani Afrika pia imeunga mkono utafiti wa awali ukionyesha wanawake ni wenye kuathirika zaidi na virusi hivyo wakiwa wajawazito.

Watafiti wanahisi mabadiliko yanayotokea kwenye mfumo wa kingamaradhi wa mjamzito huenda ikachangia kwa ongezeko la mpenzi wake kuathirika.

Shirika moja la hisani Uingereza limesema matokeo hayo yameonyesha umuhimu wa kujipima kabla ya kujifungua.

Matokeo ya utafiti huo yamewasilishwa katika mkutano wa kimataifa wa vijiumbe maradhi huko Pittsburgh, sanjari na utafiti tofauti ukionyesha dawa tepetepe ya vijiumbe maradhi ni salama kutumiwa wakati wa ujauzito kuzuia kuenea kwa virusi vya ukimwi.

Mabinti wadogo wenye umri wa kubeba ujauzito ni miongoni mwa wenye hatari ya kuambukizwa virusi hivyo kwenye nchi zenye waathirika wengi zaidi.

Hatari ya kubeba ujauzito

Mara nyingi utafiti umekuwa ukionyesha kuwa wanawake wana hatari zaidi ya kuathirika na virusi vya ukimwi kutoka kwa muathirika wakiwa wajawazito, lakini hii ni mara ya kwanza kwa watafiti kuonyesha kuwa wanaume wana uwezo wa kuathirika zaidi iwapo wenzao wana ujauzito.

Utafiti huo, uliofanywa Botswana, Kenya, Rwanda, Afrika Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia, uliwahusisha wapenzi 3,321 ambapo mpenzi mmoja alikuwa ameathirika wakati mwengine hakuwa amethirika.

Kwa upande wa wanawake, imeonekana sababu nyingine mbali na ujauzito zinachangia ongezeko la hatari ya kuambukizwa ukimwi.

Lakini kwa upande wa wanaume, uhusiano baina ya ujauzito na hatari yao ya kuambukizwa ukimwi ni wazi zaidi, hata baada ya kuangalia na sababu zengine, kama ngono zembe.

Mkuu wa utafiti huo Dr Nelly Mugo, kutoka Chuo kikuu cha Nairobi na Chuo kikuu cha Washington mjini Seattle, amesema huenda mabadiliko ya kibiolojia wakati wa ujauzito ndio humfanya mwanamke awe mwepesi kuathirika na virusi hivyo.

" Moja ya changamoto kubwa tunazokumbana nazo hapa Uingereza ni kwamba mmoja kati ya wanne wenye virusi vya ukimwi hana hata habari kuwa ana virusi hivyo, kwasababu hawajapimwa."