Amnesty: Mataifa makubwa yakiuka haki

Shirika la Amnesty limetoa ripoti yake ya kila mwaka

Shirika la kutetea haki za kibinadam la Amnesty International limeshutumu baadhi ya mataifa yenye ushawishi mkubwa duniani kwa kukiuka haki za kibinadam na kuvuruga juhudi za kimataifa za kuwatendea haki waliodhulumiwa.

Katika ripoti yake ya kila mwaka shirika hilo la amnesty limeyataka mataifa 20 tajiri duniani maarufu kama G-20 kujisajili kama wanachama wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC.

Mataifa ya Marekani, Uchina, Urusi, India na Indonesia yamekataa kutambua mahakama hiyo.

Kwa mjibu wa ripoti hii, mataifa mia moja kumi na moja yameripotiwa kuendeleza mateso dhidi ya raia wake, mataifa mengine hamsini na tano yamearifiwa kuwafungulia watuhumiwa wasio na hatia kesi zisizo kuwa za haki, huku mataifa tisini na sita yakiwazuia wanachi wake kujieleza wazi.

Pamoja na hayo shirika hilo linadai kwamba serikali zenye ushawishi mkubwa duniani zinaendelea kuvuruga juhudi za kimataifa za kuwatendea haki waliodhulumiwa.

Shirika hilo pia limesema ulegevu wa kutochukua maamuzi makali katika baraza la haki za kibinadam la Umoja wa Mataifa ni ishara kuwa jamii ya kimataifa imeshindwa kuwajibika wakati inapohitajika.

Limekashifu muungano wa Afrika kwa kutoshirikiana na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita katika kutekelezwa kwa kibali cha kukamatwa kwa rais wa Sudan Omar al Bashir, kuhusiana na uhalifu wa kivita katika eneo la darfur.

Lakini limetaja kibali hicho cha kwanza cha kukamatwa kwa rais anayehudumu kama hatua muhimu ya kuafikiwa haki na inatoa ujumbe kwamba hakuna aliyejuu ya sheria.