Mabaharia wawazidi nguvu maharamia

Somalia
Image caption Somalia

Mabaharia waliotekwa na maharamia wa kisomali kwenye meli ya biashara inayomilikiwa na raia wa Libya wamefanikiwa kuidhibiti tena meli hiyo katika ghuba ya Aden.

Jeshi la majini la Ulaya linalopambana na uharamia katika pwani ya Somalia limesema baadhi ya maharamia wanaaminiwa kuuawa wakati wa tukio hilo.

Jeshi hilo la Umoja wa Ulaya, Navfor, limesema mmoja wa mabaharia katika meli ya biashara ya MV Rim amejeruhiwa.

Wakati huo huo, meli nyingine imetekwa katika ghuba ya Aden.

Maharamia wameteka meli hiyo yenye tani 15,000, MV QSM Dubai, katika ghuba ya Aden mapema Jumatano.

Meli hiyo ina mabaharia 24 yenye raia wa Ghana, Misri, Pakistan na Bangladesh.

Meli ya kivita ya Marekani imeripoti kuona angalau haramia mmoja kwenye meli hiyo iliyotekwa akiwa na guruneti.

'Taarifa za kukanganya'

Taarifa kutoka Navfor imesema, meli ya kivita ya EU, SPS Victoria, ilipelekwa kwenye ghuba ya Aden kutoa msaada wa kitabibu kwa mabaharia wa MV Rim.

Image caption Maharamia Somalia

Imesema kulikuwa na "taarifa za kukanganya" kwamba meli hiyo ilikuwa imevamiwa tena na maharamia.

Lakini helikopta kutoka meli hiyo ya kivita ilipofika kwenye eneo la tukio, iliweza kufahamika haraka kuwa mabaharia hao waliweza kudhibiti meli hiyo.

MV Rim, yenye mabaharia wake 10 kutoka Syria ilitekwa mwezi Februari na maharamia waliodai kikombozi cha dola za kimarekani milioni tatu ili kuwaachia wakiwa salama.

Baada ya kutekwa, waandishi wanasema maharamia waliivusha meli hiyo kwenye mji wa Laasgoray, mpakani mwa miji ya Somalia inayojitawala yenyewe ya Somaliland na Puntland.

Takwimu zilizotolewa na shirika la kimataifa linalosimamia safari za majini (IMB) zinaonyesha kuwa mashambulio ya maharamia duniani yameporomoka kwa asilimia 34 katika miezi mitatu ya mwaka 2010 ukilinganisha na mwaka mmoja uliopita, kutokana na kuwepo kwa meli za kigeni kwenye ghuba ya Aden.

Takriban meli 20,000 hupita kwenye ghuba ya Aden kila mwaka, zikielekea na kurudi kutoka mfereji wa Suez.