Samantar wa Somalia kushtakiwa Marekani

Mahakama Kuu ya Marekani
Image caption Mahakama Kuu ya Marekani

Mahakama kuu ya Marekani imetoa uamuzi wa kutozuia kesi inayomkabili aliyekuwa waziri mkuu wa Somalia Mahamed Ali Samantar iliyofikishwa na watu wanaodai kuteswa naye.

Kesi hiyo iliwasilishwa na Wasomali wanaoishi Marekani chini ya sheria ya Usalama wa walioathirika kwa kuteswa ya mwaka 1991.

Awali jaji aliamua kuwa Bw Samantar ana kinga ya kidiplomasia.

Bw Samantar kwa hivi sasa anaishi katika jimbo la Virginia nchini Marekani.

Kesi hiyo inamshutumu Bw Samantar kwa kuamuru majeshi yake kuwatia kizuizini, kuwatesa, na kuua Wasomali wa koo ya Issaq.

Mahakama hiyo imesema sheria ya kinga kwa mataifa ya nje ya mwaka 1976 inalinda mataifa ya nje kutoshtakiwa katika mahakama za kimarekani, ila haiwapi kinga kwa viongozi wa zamani wa mataifa hayo.

Bw Samantar alikuwa waziri wa ulinzi wa Somalia katika miaka ya 80 na waziri mkuu tangu 1987 hadi 1990.

Somalia inaendeshwa bila ya kuwa na serikali thabit tangu wababe wa kivita walivyompindua Rais Siad Barre mwaka 1991.