Waziri Mkuu wa Kenya afanyiwa upasuaji

Image caption Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga

Daktari wa Waziri Mkuu Raila Odinga, Oluoch Olunya, amethibitisha kuwa Odinga amefanyiwa upasuaji katika ubongo wake baada ya kubainika kuwa kulikuwepo na shinikizo kubwa katika kichwa chake.

Daktari Olunya aliyekuwa akihutubia waandishi wa habari kuhusiana na kulazwa kwa Waziri Mkuu katika hospitali ya Nairobi, amesema kwamba Waziri Mkuu aliwaambia kuwa aligonga kichwa chake kwenye gari lake majuma matatu yaliyopita.

Mtaalamu huyo wa upasuaji wa ubongo amesema kuwa Odinga anaendelea kupata nafuu na kwamba ameweza kukaa kwa urahisi katika chumba chake hospitalini.

Muuguzi huyo pia amesema Raila ana uchovu mwingi mwilini na anahitaji kulazwa kwa siku tano zijazo.

Awali taarifa kutoka kwa ofisi yake ilidai kwamba alikuwa na uchovu tu.

Bwana Odinga alipelekwa hospitalini Jumatatu mchana baada ya kushiriki mkutano wa kisiasa na madaktari wake waliamuru apumzike hospitalini.

Hadi sasa Raila Odinga mwenye umri wa miaka 65 amekuwa ni mtu mkakamavu.

Katika miezi ya hivi karibuni amekuwa akipigia debe katiba mpya inayopendekezwa na hajaripotiwa kuwa na matatizo ya kiafya.

Taarifa ya kupasualiwa kwake imewashangaza wengi.

Hadi sasa , maswali mengi kuhusu afya ya kiongozi nchini Kenya yameelekezwa kwa rais Mwai kibaki.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 2003 kulikuwa na tetesi kwamba alipata kiarusi. Hata hivyo maafisa wake walikanusha madai hayo wakisema alikuwa na matatizo madogo tu ya kiafya.