Waasi Darfur wawaachia huru wanajeshi

Waasi Darfur
Image caption Waasi Darfur

Waasi katika eneo la Darfur wamewaachilia wanajeshi 35 wa serikali ambao wamekuwa wakiwashikilia baada ya machafuko kuibuka wiki iliyopita.

Msemaji wa kundi hilo la waasi la Justice and Equality Movement (JEM) wameiambia BBC kuwa wanajeshi tisa walikuwa wamejuruhiwa lakini walishugulikiwa vizuri.

Msemaji huyo ameilaumu serikali kwa kujaribu kulitisha kundi hilo.

Mapigano kati ya serikali na waasi katika eneo hilo la Darfur yalizuka upya baada ya kundi hilo la JEM kususia mazungumzo ya amani mwezi uliopita.

Waasi hao walikuwa wametia saini makubaliano ya awali ya kumaliza mapigano mwezi Februari.

Mwenyekiti wa baraza la kundi la JEM ameiambia BBC, ''Tuliheshimu makubaliano lakini serikali ya Sudan ikaanza kutushambulia, sio sisi ambao tulikiuka makubaliano,''

Watu wapatao 600 waliuawa katika mapigano hayo ya Darfur mwezi uliopita.

Idadi hiyo inasemekana kuwa kubwa zaidi tangu majeshi ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kupelekwa huko mwaka 2008.

Bw Elfaki amesema wanajeshi wa serikali walikamatwa baada ya kuwashambulia waasi hao.

Amesema, ''Tisa kati yao walijeruhiwa na hatungeweza kuwatibu, tuliomba usaidizi kutoka kwa Shirika la Msalaba Mwekundu,''

Kulingana na Umoja wa Mataifa takriban watu 300,000 wameuawa katika eneo la Darfur na wengine zaidi ya millioni 2.6 kuachwa bila makazi tangu mapigano yalipoanza mwaka 2003.

Hata hivyo serikali ya Sudan inasema idadi hiyo sio sahihi.

Rais wa Sudan Omar al-Bashir anakabiliwa na tuhuma za uhalifu wa kivita huko Darfur katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu lakini amekanusha madai hayo.