Maharamia waiachia meli ya Asian Glory

Asian Glory
Image caption Meli ya Asian Glory

Maharamia wa Kisomali wamewaachilia huru mabaharia 25 wengi kutoka mashariki mwa Ulaya pamoja na meli yao baada ya miezi sita tangu wawateke.

Wizara ya fedha ya Bulgaria imesema meli hiyo yenye bendera ya Uingereza inayosafirisha magari, Asian Glory, ilitarajiwa kuelekea Oman huku ikisindikizwa na Uingereza.

Haijajulikana hadi sasa iwapo kikombozi kimelipwa kuiachilia meli hiyo pamoja na mabaharia wake.

Maji yazungukayo Somalia ni miongoni mwa maeneo hatari duniani.

Raia 10 wa Ukraine, wanane kutoka Bulgaria, Wahindi watano na wawili kutoka Romania ndio jumla ya mabaharia katika meli hiyo ya Asian Glory, inayosimamiwa na shirika la mabaharia la Zodiac.

Zodiac imesema katika wavuti yake kwamba mabaharia wote wameripotiwa "kutodhuriwa na wako salama".

Meli hiyo yenye tani 45,000 ilitekwa kilomita 1,000 kutoka pwani ya Somalia, Januari 1.