ICC yaagiza kushikwa kwa washukiwa Sudan

Kijiji katika jimbo la Darfur
Image caption Kijiji katika jimbo la Darfur

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa anaongeza juhudi kuhusu kesi dhidi ya raia wawili wa Sudan wanaotuhumiwa kwa uhalifu wa kivita.

Luis Moreno-Ocampo amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuiamuru Khartoum kuwakabidhi wanaume hao kwa mahakam hiyo.

Raia hao wa Sudan walishtakiwa miaka mitatu iliyopita kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu katika jimbo la Darfur, lakini baado wanaendelea kushikilia nafasi za juu serikalini.

Watuhumiwa walishtakiwa kwa mashambulizi katika vijiji kadhaa huko Darfur, ambayo yalisababisha mauaji ya watu wengi, ubakaji na watu kutoroka makaazi yao.

Bw Ali Kushayb ni kiongozi wa wanamgambo wanaolaumiwa kuhusika na uhalifu huo. Na Bw Ahmed Haroun, waziri wa zamani wa mambo ya ndani ambaye sasa ni mkuu wa mkoa, anashtumiwa kupanga mashambulizi hayo.

Mwezi uliopita majaji wa Mahakama ya ICC walitangaza kuwa serikali ya mjini Khartoum haiwajibiki ipasavyo kuwakabidhi watuhumiwa hao.

Sasa mwendesha mashtaka mkuu, Bw Ocampo alilihimiza Baraza la Usalama kushinikiza kwa nguvu ili kuhakikisha kukamatwa kwa watu hao.

Akijibu wito huo, Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, Abdalmahmoud Abdalhaleem alimshtumu Bw Ocampo kwa kuwa na malengo yanayochochewa kisiasa, na kusema mpango huo unalenga kutatiza juhudi za amani katika jimbo la Darfur.

Bw Ocampo alisema mashambulizi dhidi ya raia yanaendelea kwa kiwango kikubwa Darfur, licha ya taarifa kusema kuwa hali imeimarika.