Japan yailaza Cameroon

Image caption Keisuke Honda,wa pili kulia, aliyefunga bao la Japan dhidi ya Cameroon, kwenye mchuano wa kundi E, Kombe la Dunia 2010

Japan imeishinda Cameroon bao 1-0 katika uwanja wa Free State mjini Bloemfontein, mechi ya kundi la E kwenye michuano ya Kombe la Dunia.

Bao la Japan lilifungwa na Keisuke Honda katika dakika ya 38 kufuatia kizazaa kwenye lango la Cameroon.

Pasi iliyotolewa na kiungo wa Japan Daisuke Matsui iliwazidi kimo Nocolas Nkoulou na Stephane Mbia , mpira ukakaribia lango na hapo ndipo Honda ambaye anaichezea klabu ya CSKA Moscow alipomalizia kwa kufunga bao.

Stephane Mbia alikaribia kusawazisha katika kipindi cha pili lakini kwaju lake likagonga mwamba.

Mshambuliaji wa Cameroon alidhibitiwa na walinzi wa Japan, na alifanya jaribio moja tu katika kipindi cha pili baada ya kuichenga safu ya ulinzi, akatoa pasi kwake Choupo- Moting ambaye alipaisha mpira.

Awali katika kundi hilo la E Uholanzi iliishinda Denmark mabao 2-0 katika uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg.

Denmark walijifunga bao la kwanza kupitia Simon Paulson, naye mchezaji wa Klabu ya Liverpool Dirk Kuyt akaifungia Uholanzi bao la pili.

Miongoni mwa timu 6 za Afrika zinazoshiriki michuano hiyo ya Kombe la Dunia, hadi sasa ni Ghana tu waliopata ushindi baada ya kuwafunga Serbia bao 1-0 siku ya Jumapili.

Afrika Kusini walitoka sare moja kwa moja na Mexico katika mechi ya ufunguzi, Nigeria ikashindwa 1-0 na Argentina ilhali Algeria wakafungwa 1-0 na Slovenia.

Siku ya Jumanne timu nyingine kutoka Afrika- Ivory Coast itacheza dhidi ya Ureno, mechi ya kundi G,mjini Port Elizabeth.

Bado hakuna uhakika wa mshambuliaji wa Ivory Coast Didier Drogba kucheza, baada ya kupata jeraha kwenye mechi ya kirafiki.