Viongozi wawili wakamatwa Kenya

Image caption Mwathirika wa mlipuko abebwa hospitali ya Kenyatta,Nairobi.

Polisi nchini Kenya wamemkamata naibu waziri na mbunge mmoja kwa kutoa kauli za chuki katika kampeni ya katiba mpya, baada ya tukio la Jumapili ambapo watu sita walifariki dunia baada ya mlipuko wa guruneti mjini Nairobi.

Naibu waziri wa Barabara Wilfred Machage na Fred Kapondi ni miongoni mwa wabunge sita, akiwemo waziri wa Elimu ya Juu William Ruto, anayeshutumia kwa kutoa kauli hizo.

Wote sita wamekana kuhusika na madai hayo.

Watu hao walikufa baada ya kushambuliwa na guruneti katika mhadhara wa kidini kwenye mji mkuu, Nairobi, iliyoandaliwa na upande wanaopinga katiba wanaojulikana kama "No".

Viongozi wa dini wameishutumu serikali, inayopinga kampeni ya kuunga mkono katiba mpya wajulikanao kama "Yes", kwa kuhusika na mashambulio hayo.

Mwandishi wa BBC, Will Ross mjini Nairobi amesema, Wakenya wengi wanatilia wasiwasi madai ya viongozi hao wa kanisa ya kuwa serikali inahusika na mlipuko wa Jumapili, hasa inavyoonekana kuwa wengi tayari wanaonekana kuiunga mkono kampeni ya "Yes".

' Kusimamisha kampeni'

Siku ya Jumatatu waziri mkuu Raila Odinga alisema shambulio hilo lilikuwa linafanyiwa uchunguzi na kutoa wito wa kuacha kushuku nani kahusika mpaka uchunguzi utakapokamilika.

Wabunge wengine watano wanaoshutumiwa kutoa kauli za chuki wanatarajiwa kujibu mashtaka hayo mbele ya tume ya taifa ya mshikamano na uadilifu (NCIC) siku ya Jumanne.

Kulingana na ripoti kutoka gazeti la Daily Nation, tume hiyo pia imemwandikia Rais Mwai Kibaki na Bw Odinga, wakiomba kusimamishwa kwa kampeni zote za katiba, kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni iliyopangwa kufanyika Agosti.

Baadhi wanahofia kurejea kwa ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi wa Desemba 2007, iliyosababisha vifo vya takriban watu 1,300 na 300,000 wakibaki bila makazi.

Ghasia hizo zilichochewa zaidi na ugomvi wa ardhi baina ya makabila yanayopingana na rasimu hiyo ya katiba inatarajia kuunda tume ya kushughulikia masuala ya ardhi ya umma na inayomilikiwa na jamii, ambayo nayo imepingwa na baadhi ya watu.

Vurugu hizo zilimalizika baada ya wapinzani wa uchaguzi huo Bw Kibaki na Bw Odinga kukubali kugawana madaraka na kuandika katiba mpya.