Sudan yatangaza baraza jipya la Mawaziri

Rais Omar Al Bashir

Baraza jipya la mawaziri wa serikali ya muungano nchini Sudan litaapishwa hii leo. Baraza hilo lililotangazwa na rais Omar Al Bashir hapo jana lina jumla ya mawaziri 77, saba kati yao wakiwa wanawake.

Chama cha Sudan Kusini SPLM kimepewa wizara muhimu ya mafuta. Rais Bashir ameteuwa baraza hili kufuatia ushindi wake mwezi Aprili ambao ulipingwa na vyama vya upinzani.

Serikali hii mpya inatarajiwa kuwa ya mwisho kabla ya kufanyika kura ya maoni kuhusu kujitenga kwa eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Sudan Kusini hapo mwakani.

Baraza hili linajumuisha mawaziri kutoka chama cha Bw. Bashir cha National Congress Party{NCP} kikiwakilisha Sudan Kaskazini na SPLM ya Sudan Kusini.

Rais Omar Al Bashir amegawa wizara ya kawi katika idara tatu ikiwa ni pamoja na mafuta, madini na umeme.

Wizara ya mafuta itasimamiwa na Lwal Akwek Deng wa chama cha SPLM. Chama hicho kinachotawala eneo la kusini kimetengewa nafasi 35 za uwaziri.

Hatua hii ya kukipa SPLM wizara muhimu imetajwa na wadadisi kama ya kuwashawishi raia wa Sudan Kusini kutounga mkono kura ya kujitenga na eneo la Kaskazini.

Kura hii ya maoni ni mojawapo na makubaliano kwenye mkataba wa amani ulioafikiwa na mwaka 2005 ili kumaliza vita vya miongo miwili kati ya Sudan Kaskazini na Kusini.