Marekani na Slovenia zatoka sare

Michael Bradley
Image caption Michael Bradley (wa pili kushoto) wa Marekani afunga goli la pili baada ya kipa wa Slovenia Samir Handanovic kushindwa kuuzuia

Michael Bradley alifunga bao la dakika za mwisho lililoiwezesha Marekani kutoka sare na Slovenia mabao 2-2 kwenye mchuano wa kundi C, katika uwanja wa Ellis Park mjini Johannesburg.

Kipindi cha kwanza kilimalizika Slovenia wakiongoza mabao 2-0, na wakionekana kujipatia nafasi ya raundi ya pili ya michuano hiyo ya Kombe la Dunia.

Mabao hayo yalifungwa na Valter Birsa na Zlatan Ljubijankic.

Mwanzo wa kipindi cha pili kocha wa Marekani Bob Bradley alifanya mabadiliko mawili yaliyoleta matunda.

Landon Donavon alifunga bao la kwanza la Marekani dakika 3 tu baada ya kipindi cha pili kuanza, na bao la pili likafungwa katika dakika ya 82 na Michael Bradley, mwanawe kocha wa Marekani.

Refa kutoka Mali Koman Coulibaly alikataa kile kilichoonekana kuwa bao la 3 la Marekani lililokuwa limesukumwa wavuni na Maurice Edu, kutokana na kosa la mchezaji wa Slovenia kusukumwa.

Slovenia ambayo katika mechi ya ufunguzi iliifunga Algeria bao 1-0 ina pointi 4 katika kundi hilo la C, nayo Marekani ina pointi 2 baada ya kutoka sare na England kwenye mechi yao ya kwanza.