Kenya yasajili namba za simu za mkononi

Image caption Mtumiaji wa simu ya mkononi

Kenya imeanza kusajili namba zote za simu za mkononi kwa nia ya kupunguza uhalifu nchini humo.

Watumiaji wa simu watatakiwa kuonyesha vitambulisho na ushahidi wa anuani ya mahala wanapoishi.

Serikali imesema, namba yeyote itakayokuwa haijsajiliwa ifikapo mwisho wa mwezi Julai itafungwa.

Mwandishi wa BBC Odhiambo Joseph mjini Nairobi amesema watu wengi wameonekana kuunga mkono hatua hiyo, wakiwa na matumaini ya kupunguza uhalifu.

Amesema, magenge ya watekaji nyara aghlabu hutumia namba zisizosajiliwa kudai kikombozi.

Kamishna wa polisi Mathew Iteere ameiambia BBC simu za mkononi lazima zisajiliwe kwani siku hizi huweza kutumika kama kompyuta.

"Imekuwa chombo cha benki, inaweza kutumika kuiba taarifa, kutuma maelezo yasiyoruhusiwa na makosa ya udanganyifu."

Wiki iliyopita afisa wa wizara ya habari Bitange Ndemo alisema kusajili namba hizo kutasaidia mamlaka husika kupambana na ugaidi, biashara haramu ya dawa za kulevya, pamoja na kujua wanaotuma ujumbe wenye chuki.

Nchi jirani ya Tanzania imeshaanza kutumia mfumo huo, kwahiyo mwandishi wetu anasema haina utata wowote.

Amesema eneo aliloenda kulitembelea lilikuwa limejaa watu waliokuwa wakisajili namba zao.

Kenya ina takriban watumiaji milioni 20 wa simu za mkononi, karibu nusu ya idadi ya raia wote nchini humo, na ina mfumo mzuri sana wa huduma za benki kupitia simu za mkononi.