Majeshi ya kutunza amani yauawa Darfur

Askari wa kutunza amani Darfur, Sudan
Image caption Majeshi ya kutunza amani Darfur, Sudan

Askari watatu wa Rwanda wa vikosi vya kutunza amani wameuawa katika jimbo la Darfur la Sudan.

Kwa mujibu wa maafisa wa jeshi hilo wanajeshi walishambuliwa magharibi mwa Darfur ambako walikwenda kutoa ulinzi kwa kambi mpya inayojengwa katika eneo lililowahi kushambuliwa siku za nyuma.

Umoja wa mataifa unakisia kuwa watu 300,000 wameuawa mjini Darfur tangu waasi waanze mashambulio yao mnamo mwaka 2003.

Msemaji wa vikosi vya muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa Kemal Saiki ameliambia shirika la habari la AFP kuwa watu 20 waliokuwa na bunduki za "AK47s waliwashambulia wanajeshi hao.

Alisema hajui ni kundi gani kati ya makundi kadhaa ya wapiganaji wa Darfur kilihusika.

Wanajeshi 27 wa kikosi cha kutunza amani kinachojulikana kama Unamid wamekufa tangu Umoja wa Mataifa kushika udhibiti wa eneo hilo mwaka 2008.

Baada ya kipindi cha utulivu, idadi ya vifo vya raia imeongezeka Darfur.

Takriban watu 600 wamekufa katika mapigano ya Darfur mwezi uliopita, hii ikiwa ni idadi kubwa ya vifo kwa kipindi cha mwezi mmoja tangu mwaka 2008.