Cyprus yazuia 'meli ya silaha ya Sudan'

Image caption Meli ya Santiago

Cyprus imeizuia meli iliyobeba vifaa vya kijeshi kuondoka hadi wakaguzi wathibitishe mzigo wao haukiuki vizuizi vya silaha vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya.

Waziri wa biashara Antonis Paschalides ameiambia redio ya Cyprus kulikuwa na "vifaa visivyoruhusiwa" katika meli hiyo ya Santiago, kama vile mabomu na vifaa vya kijeshi.

Hati ya meli hiyo inaonyesha ilikuwa inaelekea Sudan na Singapore.

Umoja wa Ulaya umepiga marufuku usafirishaji wa silaha kuelekea Sudan, huku Umoja wa Mataifa ukiweka kizuizi cha silaha kwa makundi ya wapiganaji mjini Darfur.

Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe baina ya kaskazini na kusini tangu miaka ya 1960 imesababisha vifo vya takriban watu milioni 1.5.

Wakati huo huo, mapigano yanayoendelea Darfur yamesababisha zaidi ya watu milioni 2.6 kuhama makazi yao na vifo vya watu 300,000.