Kenya yafungua mahakama ya maharamia

Serikali ya Kenya imefungua mahakama maalum itakayotumiwa kuendesha kesi za washukiwa wa uharamia. Mahakama hiyo imefunguliwa katika gereza la Shimo la Tewa, mjini Mombasa katika pwani ya Kenya.

Jumla ya washukiwa 106 wanazuiliwa katika gereza hilo wakisubiri kukamilishwa kwa kesi zao. Maharamia wengine 18 tayari wamehukumiwa na wanatumikia vifungo vyao katika gereza la Shimo la Tewa.

Mahakama hiyo maalum inagharimiwa na ofisi ya umoja wa mataifa inayoshughulikia uhalifu. Serikali kadhaa zikiwemo Marekani, Ufaransa, Canada na Ujerumani zinafadhili shughuli hiyo. Tayari ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa inasema imeipa serikali ya Kenya dola milioni 5.

Hapo awali serikali ya Kenya ilikuwa imetishia kusitisha mpango wa kuwakubali maharamia walioshikwa katika bahari ya Hindi, ikidai kuwa jamii ya kimataifa haikuwa inasaidia kulipia gharama za kuwazuilia na kuendesha kesi za washukiwa hao.

Jamii ya kimataifa imeelezea imani kuwa kufunguliwa kwa mahakama hiyo maalum kutasaidia kuendesha upesi kesi za uharamia na hivyo kusaidia kukabiliana na uharamia katika bahari ya Hindi.