Wakongo wajitokea kumzika Chebeya

Floribert Chebeya
Image caption Floribert Chebeya

Mamia ya waombolezaji wamehudhuria mazishi ya mtetezi mkuu wa haki za binadamu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Floribert Chebeya, aliyeuliwa mapema mwezi huu.

Zaidi ya watu elfu moja, akiwemo waziri wa sheria na haki za binadamu wa nchi hiyo, Bambi Luzolo, pamoja na mabalozi wa mataifa ya nchi za magharibi, walihudhuria ibada katika kanisa moja mjini Kinshasa.

Floribert Chebeya alipatikana akiwa ameuawa ndani ya gari lake mwanzoni mwa mwezi huu.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Congo yalitaka maziko yafanyike siku ya kimataifa ya kuwakumbuka walionyanyaswa na kuteswa, ili wengi waweze kumkumbuka vyema Chebeya.

Bw Chebeya aliongoza kampenzi za kutetea haki za binadamu nchini Congo, kwa muda wa miongo mitatu iliyopita.

Licha ya kutaka uchunguzi huru ufanyike kufuatia kifo chake, tume moja ya kijeshi imepewa jukumu hilo.

Viongozi kadhaa wa upinzani walikusanyika nje ya kanisa, wakitaka Rais Joseph Kabila ajiuzulu.