Nchi tajiri zatakiwa kutekeleza ahadi zake za misaada

Wakuu wa G8

Katika Mkutano wa mataifa nane tajiri zaidi duniani G8 unaofanyika mjini Toronto Canada, Marekani na Uingereza zimezitaka nchi nyingine kutekeleza ahadi za misaada zilizotoa katika kikao cha awali kilichofanyika nchini Uscoti mwaka 2005.

Wakati huo ahadi zilitolewa kwa lengo la kuinua bajeti ya misaada kwa kiwango cha walau dola bilioni hamsini kufikia mwaka 2010, Lakini kundi hilo limeweza kutoa dola bilioni ishirini pekee.

Marekani, Uingereza na Canada walitekeleza ahadi zao, lakini Japan, Ufarasa na Ujerumani hazikukamilisha ahadi zao, na Italy haikutekeleza kabisa ahadi zake za msaada wa fedha.

Viongozi wa G8 pia wanakabiliwa na shinikizo la kufikia malengo ya Maendeleo ya Milenia, ambayo yanajumuisha lengo la kupunguza viwango vya vifo vya akina mama na watoto wanaozalia.

Canada sasa imeahidi kutoa dola bilioni tatu kwa kipindi cha miaka mitano ili kutekeleza ahadi hii.

Hata hivyo nchi zinazoendelea zinasema bado pesa hizo hazitoshelezi kiwango cha matatizo yaliyopo.