Uchaguzi wa kidemokrasia wafanywa Guinea

Uchaguzi Guinea
Image caption Upigaji kura Guinea

Wananchi wa Guinea wamepiga kura katika uchaguzi huru wa kwanza kuwahi kufanyika tangu nchi hiyo kujipatia uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka 1958.

Raia walijitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi huo wa kihistoria.Ripoti zinasema kulikuwa na milolongo mirefu ya wapiga kura katika vituo mbalimbali.

Kiongozi wa serikali ya mpito ya nchi hiyo Jenerali Sekouba Konate amesema wanajeshi hawakuruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi huo.

Jumla ya watu 24 wanagombea nafasi ya urais.

Guinea imekuwa ikiongozwa na utawala wa kijeshi. Jeshi lilianza kuongoza mwaka 2008 baada ya kifo cha aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Lansana Conte ambaye aliongoza kwa zaidi ya miongo miwili.

Machafuko yalitokea Septemba mwaka jana, baada ya majeshi kushambulia waandamanaji katika mji mkuu Conakry na kusababisha vifo vya watu 150.

''Uchaguzi umefanyika kwa njia ya amani na kuna hali ya matumaini,'' alisema Yakubu Gowon ambaye anaongoza kikosi cha waangalizi kutoka shirika la haki za binadamu la Carter Center lenye makao yake Marekani.

Bw Gowon amekadiria kuwa idadi ya watu waliojitokeza ni kati ya asilimia 75 na 80.

Katika nchi jirani ya Liberia ambako kuna idadi kubwa ya raia wa Guinea ambao walikimbilia nchini humo baada ya vita, pia walipiga kura mjini Monrovia.

Ushindani mkali uko kati ya Mawaziri Wakuu wa zamani Cellou Dalein Diallo na Sidya Toure na mwanasiasa mkongwe Alpha Conde.

Licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa madini Guinea imesalia kuwa mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani.

Matokeo ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutolewa katika muda wa siku chache zijazo.

Iwapo hakuna mgombea atakayepata ushindi wa wazi, duru ya pili ya uchaguzi itafanyika tarehe 18 Julai 2010.