Burundi kufanya uchaguzi wa urais bila upinzani

Raia wa Burundi wanachagua rais  bila upinzani

Raia wa Burundi wanapiga kura katika uchaguzi wa urais ikiwa ni wazi kuhusu anayetazamiwa kutwaa ushindi.

Hii ni baada ya vyama vya upinzani kuwaondoa wagombea wake na kumuacha kiongozi wa sasa Pierre Nkurunziza akiwa mgombea wa pekee.

Uchaguzi huu ndiyo wa kwanza tangu serikali na kundi la mwisho la waasi FNL kuafikiana mkataba wa amani . Kundi hilo liliitikia kushiriki katika mpango wa kisiasa nchini humo.

Hata hivyo wadadisi wameonya kwamba nchi hiyo inakabiliwa na tisho la kurejelea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.Mwezi jana chama tawala kilitwaa ushindi kwenye uchaguzi wa mabaraza uliosifiwa na waangalizi wa kimataifa.

Hata hivyo makundi ya upinzani yalilalamikia udanganyifu hali iliyopelekea muungano wa vyama vya upinzani kutangaza kujiondoa kwenye mchuano wa urais.Mpinzani mkuu wa rais Nkurunziza Agathon Rwasa ametoroka nchini na anadaiwa kukimbilia mafichoni katika nchi jirani ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Katika kipindi kizima cha kampeini misururu ya milipuko ya gruneti ndiyo iliyotawala ambapo watu watano walipoteza maisha na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa. Matukio haya yanatilia shaka mstakabali wa mkataba wa amani uliosainiwa mwaka 2006.