Wakimbizi wa Rwanda wahofia kurejea nyumbani

paul Kagame rais wa Rwanda

Ripoti ya Shirika la kimataifa linalowashughulikia wakimbizi {UNHCR} nchini Uganda imesema miaka 16 tangu kutokea mauaji ya kimbari nchini Rwanda,Maelfu ya Wanyarwanda waliokimbia mauaji hayo wangali na hofu ya kurejea nyumbani.

Taarifa hiyo ya UNHCR imesema licha ya kuwashawishi wakimbizi hao, kurejea nyumbani wameendelea kusisitiza kusalia Uganda

Wakimbizi wanaohofia kurejea nyumbani ni kutoka jamii ya Wahutu,wanakotoka wanamgambo waliolaumiwa kutekeleza mauaji ya raia laki nane wengi kutoka jamii ya Watutsi.

Wakimbizi hao wanasema serikali ya Rwanda imeendelea kuwabagua watu kutoka jamii yao.

Ripoti hii imetokea wakati shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights watch limelalamikia serikali ya Rwanda kwa kuendelea kuwakandamiza wapinzani wake kabla ya uchaguzi mkuu mwezi Agosti.

Hii ni kufuatia mauaji ya mwandishi habari ambaye alipigwa risasi nje ya makaazi yake wiki jana.

Mwandishi habari huyo amekuwa akichunguza jaribio la mauaji dhidi ya jenerali wa jeshi la Rwanda mapema mwezi huu nchini Afrika Kusini.

Serikali ya Rwanda imekanusha kuhusika na visa hivyo ikisema matukio hayo yanatumiwa kuharibia sifa utawala wa Kigali.