Robo fainali ya kukata na shoka

Image caption Brazil imewafunga Chile mabao 3-1

Robo fainali ya kwanza ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini itakutanisha mabingwa mara tano Brazil na Uholanzi siku ya Ijumaa mjini Port Elizabeth, baada ya timu hizo kufuzu kufuatia ushindi wa Jumatatu.

Brazil iliendelea kudhihirisha azma yake ya kulitwaa kombe hilo kwa mara ya sita ilipowafunga Chile mabao 3-0 katika uwanja wa Ellis Park mjini Johannesburg.

Awali katika uwanja wa Moses Mabhida mjini Durban, Arjen Robben na Wesley Sneider walifunga mabao yaliyoiwezesha Uholanzi kuishinda Slovakia 2-1 na hivyo kujiandikishia nafasi miongoni mwa nane bora.

Mabao ya Brazil dhidi ya Chile yalipatikana kupitia mlinzi Juan aliyefunga kwa kichwa katika dakika ya 38, kabla ya Luis Fabiano kuongeza la pili dakika 4 baadaye.

Robinho alifunga bao la tatu na la ushindi kwa Brazil katika dakika ya 59 kufuatia pasi kutoka Ramires.

Image caption Wesley Sneijder

Uholanzi walionekana kuelekea kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Slovakia hadi muda wa ziada, wakati mlinda mlango Maarten Stekelenburg alipomwangusha Martin Jakubo kwenye eneo la hatari, na hivyo Slovakia wakapata penalti iliyofungwa na Robert Vittek.

Uholanzi haijapata kushinda Kombe la Dunia na imeshafikia hatua ya fainali mwaka 74 na 78, na wakati huu wanajitahidi kutimiza hamu ya kutwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza.

Robo fainali nyingine siku ya Ijumaa itakuwa kati ya Ghana na Uruguay katika uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg, hii ikiwa ni mara ya tatu katika historia ya Kombe la Dunia kwa timu kutoka Afrika kufikia hatua ya nane bora.

Siku ya Jumamosi itafanyika robo fainali ya tatu kati ya Ujerumani na Argentina katika uwanja wa Green Point mjini Cape Town.

Timu zitakazochuana kwenye robo fainali ya mwisho zitafahamika Jumanne, baada ya mechi za mwisho za raundi ya pili, Paraguay ikicheza dhidi ya Japan mjini Pretoria huku Uhispania na Ureno zikipambana mjini Cape Town.