Waziri Mkuu wa Kenya alazwa hospitalini

Image caption Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga

Hadi sasa Raila Odinga mwenye umri wa miaka 65 amekuwa ni mtu mwenye nguvu.

Katika miezi ya hivi karibuni amekuwa akipigia debe katiba mpya inayopendekezwa na hajaripotiwa kuwa na matatizo ya kimwili.

Kwa hiyo taarifa iliyotolewa hii leo na msemaji wake imewashangaza wengi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo madaktari wameamuru Odinga alazwe hospitalini kwa muda wakisema tu kwamba ana uchovu. Cha kukanganya ni kwamba taarifa hiyo iliwanukuu madaktari hao pia wakisema Odinga ana uwezo wa kufanya kazi kama kawaida ikiwa atajisikia kufanya hivyo. Japo hawatamruhusu kufanya hivyo.

Hadi sasa, maswali mengi kuhusu afya ya kiongozi nchini Kenya yameelekezwa kwa Rais Mwai kibaki ambaye baada ya uchaguzi wa mwaka 2003 kulikuwa na tetesi kwamba alipata kiarusi.

Hata hivyo maafisa wake walikanusha madai hayo wakisema alikuwa na matatizo madogo tu ya kiafya.