Wabunge Kenya wajiongezea mishahara

Bunge la Kenya
Image caption Bunge la Kenya

Wabunge nchini Kenya wameidhinisha nyongeza ya mishahara yao ambao utawafanya kuwa miongoni mwa wanasiasa wanaolipwa mishahara minono kabisa duniani.

Chini ya sheria mpya, waziri mkuu wa nchi hiyo atalipwa zaidi ya theluthi ya mwenzake wa Uingereza.

Atakuwa na kipato cha karibu zaidi ya asilimia 10 na anacholipwa Rais wa Marekani. Waandishi wanasema suala hilo limeibua hasira miongoni mwa wananchi na waandishi wa habari.

Wabunge wamepiga kura ili walipwe dola za kimarekani 44,000 kwa mwaka.

Lakini marupurupu ya ziada yanaweza kuongeza mshahara ukafikia dola 126,000 baada ya kukatwa kodi, ambalo ni ongezeko la asilimia 18.

Marupurupu hayo ni pamoja na dola 370 kwa kuhudhuria tu kikao cha bunge kwa siku.

Wastani wa mapato ya mwaka nchini Kenya ni takriban dola za kimarekani 730, huku wengi wa raia nchini humo wakiwa na kipato cha chini ya dola moja kwa siku.

Iwapo itapitishwa, sheria hiyo itaanza kutekelezwa wakati wa bunge lijalo, linalotarajiwa kuanza miaka miwili ijayo.

Mwandishi wa BBC wa Afrika Mashariki Peter Greste amesema majadiliano ya wabunge hao yalifanyika haraka kuliko ilivyo kawaida.

Mbunge mmoja alielezea nyongeza hiyo kuwa njia mojawapo ya kurudisha heshima katika siasa.

Hata hivyo, wachambuzi wanasema ni siku chache tu zilizopita benki ya dunia ilielezea bunge la Kenya kuwa ni mojawapo ya mabunge yaliyokita kwa vitendo vya ufisadi duniani.