Odinga akemea mishahara ya wabunge Kenya

Image caption Rais wa Kenya Mwai Kibaki na waziri mkuu Raila Odinga

Waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga amewakosoa vikali wabunge kwa kupiga kura ya kujiongezea mshahara mikubwa.

Iwapo pendekezo hilo litapitishwa, inamaanisha kila mmoja atapata malipo ya dola za kimarekani 126,000 baada ya kukatwa kodi, hivyo kuwa miongoni mwa wanasiasa wanaolipwa kiwango kikubwa cha fedha duniani.

Bw Odinga amesema muda mfupi baada ya kutolewa hospitali, " Si sawa. Inatoa ishara mbaya kwa raia wa nchi hii."

Wiki iliyopita alifanyiwa upasuaji wa kuondosha maji mazito 'ugiligili' kwenye ubongo.

Kura hiyo iliyopigwa na wabunge imeamsha hasira kubwa miongoni mwa umma.

Licha ya watunga sheria kupitisha kuongezeka kwa malipo hayo kwa asilimia 18 wiki iliyopita, bunge linatarajiwa kulijadili suala hilo siku ya Jumanne.

Vyanzo vya habari vimeiambia gazeti la Kenya Daily Nation uwezekano mkubwa ni kuwa mawaziri watalikataa pendekezo hilo.

Bw Odinga amesema ameridhika na mshahara wake wa sasa na kuwasihi wabunge wajadili mambo mengine.

Katika pendekezo hilo lililotolewa, mshahara wa waziri mkuu utaongezeka kufikia dola za kimarekani 40,000 kwa mwezi, ambayo ni theluthi zaidi ya mshahara wa waziri mkuu wa Uingereza na asilimia 10 zaidi ya Rais wa Marekani.

Hata hivyo, utekelezaji hautoanza mpaka bunge lijalo, ambapo hata nafasi ya uwaziri mkuu huenda ukawa umefutwa iwapo katiba mpya itapitishwa katika kura ya maoni mwezi Agosti.

Mshahara wa wabunge hao utakuwa dola za kimarekani 44,000 kwa mwaka. Lakini pia wana marupurupu chungu nzima, ikiwemo dola 370 kwa siku kwa kujitokeza tu bungeni.

Mapato ya mwaka kwa wastani nchini Kenya ni takriban dola za kimarekani 730, huku wengi nchini humo wakitumia kipato cha chini ya dola moja kwa siku.

Bw Odinga aliondoka hospitalini siku ya Jumapili na ameambiwa asianze kazi mpaka baada ya wiki mbili.

Alishika nyadhifa ya uwaziri mkuu miaka miwili iliyopita alipojiunga na serikali ya kugawana madaraka iliyoundwa ili kumaliza ghasia za kisiasa zilizoendelea kwa miezi kadhaa baada ya wafuasi wake kusema alifanyiwa hila katika uchaguzi wa Desemba 2007.