Nigeria 'yasalimu amri kwa Fifa'

Wachezaji wa Nigeria
Image caption Wachezaji wa Nigeria

Kwa mujibu wa ripoti kutoka Nigeria, serikali ya nchi hiyo imebatilisha uamuzi wake wa kuizuia timu ya soka ya taifa ya nchi hiyo kushiriki mashindano yote ya kimataifa.

Taarifa hizo zimetolewa saa moja kabla ya kufikia muda wa mwisho uliowekwa na shirikisho la soka duniani Fifa la kubatilisha uamuzi huo.

Fifa ilisema itaifungia Nigeria kushiriki mashindano ya soka duniani iwapo serikali ingeonekana kuingilia.

Wiki iliyopita Rais Goodluck Jonathan alisema baada ya timu hiyo kuonyesha kiwango duni katika Kombe la Dunia watazuia kushiriki mashindano yeyote ya soka kwa miaka miwili.

Siku ya Jumapili, maafisa waandamizi wawili wa shirikisho la soka la Nigeria (NFF) walifukuzwa katika hatua ya kumtuliza Rais huyo.

Chanzo cha habari kimeiambia BBC kuwa kufukuzwa kwao hakujabadili uamuzi wa Rais huyo, lakini NFF liliomba kuzungumza naye Jumatatu kwa mazungumzo ya dharura kabla ya siku hiyo waliopewa na Fifa kuwadia.