Mnigeria akutwa na maiti za watoto 70

Nigeria
Image caption Nigeria

Mtu mmoja aliyekuwa amebeba mifuko yenye zaidi ya maiti ya watoto wachanga 70 amekamatwa Nigeria.

Alikuwa ameajiriwa na chuo kikuu cha hospitali inayotoa mafunzo ya afya mjini Lagos ya kupeleka maiti makaburini.

Inadaiwa mfanyakazi huyo alikuwa akijaribu kutupa maiti hao kwani hakuwa na uwezo wa kulipa gharama za kuzikia.

Msemaji wa hospitali amesema wanashirikiana na polisi kufanya uchunguzi wa tukio hilo.

Mwandishi wa BBC mjini Lagos amesema familia nyingi hazina uwezo kabisa wa kushughulikia maiti za watoto na wengine hawana uwezo wa kulipia mahali pa kuhifadhia maiti, hivyo huwatelekeza nje ya hospitali.

Hospitali hukodisha kampuni maalum kwa ajili ya kuzika maiti hao.

'Aibu'

Afisa uhusiano wa polisi mjini Lagos Frank Mba, alisema uchunguzi wa polisi wa awali pia ulisababisha kukamatwa kwa baadhi ya wafanyakazi wa idara ya sayansi inayohusu viungo vya mwili katika hospitali hiyo inayotoa pia mafunzo.

Amesema pia mshukiwa huyo hakuwa na nia ya kutumia miili hiyo kwa matambiko.

Bw Mba alisema "Tuna uhakika mshukiwa huyo si mtu anayefanya matambiko, si muuaji na wala si mtu anayeuza viungo. Masuala mengine kama rushwa na utumiaji mbovu wa madaraka utachunguzwa."

Hospitali hiyo imeelezea tukio hilo kuwa ni la aibu kwa shirika lililohusika.

Mwandishi wa BBC Fidelis Mbah alisema watu wengi huko Lagos wameshtushwa na kutoamini kuwa hospitali hiyo yenye hadhi ya kipekee ingeweza kuruhusu kampuni hiyo kushughulikia maiti za watu bila usimamizi kutoka kwa wafanyakazi wake.