Uchaguzi wa Senate wafanyika Japan

Waziri Mkuu wa Japan Naoto Kan
Image caption Waziri Mkuu wa Japan Naoto Kan

Japan inapiga kura katika uchaguzi wa baraza la senate, uchaguzi ambao unaonekana kama kura ya maoni kwa utawala wa miezi kumi wa chama cha Democratic Party of Japan (DPJ), kinachoongozwa na Waziri Mkuu Naoto Kan.

Siku ya Jumamosi Bw Kan aliwaambia wafuasi wake kuwa Japan inapaswa kuepukana na mporomoko wa kiuchumi.

Bw Kan aliingia madarakani mwezi uliopita na kura za maoni zinaashiria kuwa chama cha DPJ na washirika wake huenda wakapoteza uwingi wa viti katika baraza hilo la senate.

Ikiwa atapata matokeo mabaya atalazimika kutafuta washirika wapya wa kisiasa, na hata kuna uwezekano wa Bw kan kuondolewa na chama chake, kama anavyosema mwandishi wa BBC mjini Tokyo Roland Buerk.

Chama cha DPJ kilishika hatamu mwezi August mwaka jana na kumaliza utawala wa nusu karne wa wapinzani wao, Liberal Democratic Party.

Bw Kan alirithi uongozi kutoka kwa Yukio Hatoyama aliyejiuzulu baada ya kuwa mamlakani kwa muda wa miezi tisa pekee.

Katika uchaguzi huu, viti 121, ambavyo ni nusu ya viti vyote vya baraza la senate vitashindaniwa.

Wakati huu, chama cha DPJ na mshirika wake, People's New Party, wana viti 122 katika baraza hilo.

Lakini kura za maoni zinaonyesha kuwa DPJ huenda kikapoteza baadhi ya viti hivyo.

Kampeni za uchaguzi zimetawaliwa na mapendekezo ya waziri mkuu kuwa Japan inahitaji kujadili uwezekano wa kupandisha kodi ya mauzo, suala ambalo limewagawa wapiga kura, kulingana na mwandishi wa BBC.

Kiasi cha raia millioni 104 wa Japan wana haki ya kupiga kura.