Waliokufa shambulio la bomu Uganda ni 74

Image caption Rais Yoweri Museveni akitembelea hospitali kuwajulia hali baadhi ya watu waliojeruhiwa katika mashambuliao hayo.

Idadi ya watu waliokufa katika mashambulio mawili ya mabomu yaliyotikisa wakati mashabiki wakiangalia mechi ya fainali ya Kombe la Dunia mjini Kampala huko Uganda, imeongezeka kufikia 74, maafisa wanasema.

Watu wengine 70 walijeruhiwa katika mashambulio hayo yaliyolengwa klabu ya mchezo wa raga ya Kampala na mgahawa mmoja wa vyakula vyenye asili ya Ethiopia.

Ingawa wanamgambo wa Al Shabab wamekiri kuhusika, polisi wanachunguza endapo walifanya mashambulio ya kujitolea muhanga.

Kulinda amani

Wanajeshi wa kulinda amani wa Uganda wanatumikia nchini Somalia, na al-Shabab wametishia kushambulia Kampala katika siku zilizopita.

Takriban askari 5,000 wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika kutoka Uganda na Burundi wapo Mogadishu kusaidia serikali ya mpito ambayo si imara.

Jeshi la AU nchini Somalia (Amisom) limekuwa likikabiliwa na mashambulio ya mara kwa mara kutoka kwa wanamgambo wanaodhibiti sehemu kubwa ya kusini na katikati ya Somalia.

Mashambulio yote mawili yalisababisha vifo na majeraha, ingawa watu wengi zaidi walikufa kwenye klabu ya mchezo wa raga, ambako mashabiki walikuwa wakifuatilia mechi hiyo kupitia skirini kubwa.