'Ukanda maalum wa bomu' wakutwa Uganda

Image caption Mwathirika wa milipuko ya mabomu Uganda

Maafisa wa Uganda wamesema, ukanda unaotumiwa na walipuaji mabomu wa kujitoa mhanga ambao haujalipuka umepatikana mjini Kampala baada ya shambulio la Jumapili lililotokea kwa watu waliokuwa wakitazama fainali ya Kombe la Dunia kupitia televisheni.

Wamesema kuna watu ambao idadi yao haijajulikana wamekamatwa.

Takriban watu 74 waliuawa katika milipuko miwili iliyotokea katika klabu ya raga na kwenye mgahawa.

Kundi la wapiganaji la Kisomali la al-Shabab limesema linahusika na mashambulio hayo kwasababu Uganda inaiunga mkono serikali ya Somalia mjini Mogadishu.

Msemaji wa serikali Fred Opolot amesema ukamataji ulifanyika baada ya ukanda huo kukutwa katika eneo la Makindye kusini mashariki mwa Kampala.

Polisi wamesema, ukanda huo ulikutwa kwenye mfuko mweusi kama ule unaotumika kubebea lap-top kwenye klabu ya usiku Jumatatu mchana.

Mfuko huo ulikuwa na milipuko na mabomu.

Mataifa ya watu hao waliokamatwa hayajatajwa lakini maafisa wamesema kichwa kimoja kilichopatikana karibu na eneo moja lilipotokea mlipuko huo kinaonekana kuwa cha Msomali, ambaye huenda alikuwa amejitoa mhanga.

Mkutano wa Umoja wa Afrika

Polisi wa Uganda wanasaidiwa na wachunguzi kutoka Marekani wakijaribu kutambua namna hasa ya milipuko hiyo ilivyopangwa na kulipuliwa.

Mwandishi wa BBC wa masuala ya Afrika Mashariki Will Ross amesema serikali ya Uganda iko katika shinikizo kubwa kuonyesha kuwa inaweza kuzuia tukio hilo la milipuko kutokea tena.

Umoja wa Afrika, ambao umepeleka majeshi yake ya kutunza amani nchini Somalia, inatarajiwa kufanya mkutano Kampala baadae mwezi huu na maafisa wamesema utafanyika kama ulivyokuwa umepangwa.

Uganda imeanza maombolezo ya kitaifa ya siku saba, huku bendera zikishushwa nusu mlingoti kote nchini.

Katika taarifa iliyotolewa mjini Mogadishu siku ya Jumatatu, msemaji wa al-Qaeda anayeshirikiana na kundi la al-Shabab, Sheikh Ali Mohamud Rage, ametishia kufanya mashambulio zaidi nchini humo.

Bw Rage alisema, " Al-Shabab wamehusika na milipuko hiyo miwili Uganda."

Waandishi wamesema idara za usalama eneo hilo sasa zitakuwa zinatathmini upya namna ya kujilinda kutoka jeshi lililothibitisha kuwa na nia na uwezo wa kushambulia nje ya mipaka ya Somalia.

Bw Rage alirudia vitisho vya kushambulia Burundi mara kadhaa, ikiwa ni nchi nyingine iliyopeleka majeshi yake Somalia.

Serikali ya Kenya imesema imeimarisha usalama katika mpaka wa Somalia.

Kenya ni washirika wa karibu na serikali ya Somalia na inawasaidia kutoa mafunzo ya kijeshi.