Mwili wa mpinzani wapatikana Rwanda

Rais Paul Kagame
Image caption Rais Paul Kagame

Mwili wa kiongozi wa upinzani nchini Rwanda aliyetangazwa kuwa amepotea umepatikana.

Chama cha Democratic Green kimesema kuwa Andre Kagwa Rwisereka amepatikana karibu na gari lake huku kichwa chake kikiwa kimening'inia.

Chama chake kimeshindwa kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa Rais unaotazamiwa kufanyika mwezi ujao.

Mashirika ya kupigania haki za binadamu yameilaumu serikali ya Rwanda kwa kukuvibana vyama vya upinzani kabla ya upigaji kura.

Mwenyekiti wa chama cha Green Frank Habineza ameiambia BBC, '' Tunaitaka serikali ya Rwanda itumie kila njia inayowezekana kupeleleza kilichosababisha kifo hiki.''

Bw.Habineza amesema mwili wa marehemu umepatikana umbali wa kilomita tatu kutoka mji wa Butare, eneo ambako gari lake lilipatikana.

Msemaji wa polisi amethibitisha kifo hicho lakini amependekeza huenda ujambazi ndio sababu kuu.

Msemaji wa polisi, Eric Kayiranga amesema ''Waliomuona usiku huo kabla ya kufariki dunia wanasema alikuwa na pesa nyingi.

Mwezi uliopita, aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Rwanda, Lt.Generali Faustin Kayumba Nyamwasa, alipigwa risasi akiwa Afrika ya kusini, majuma machache baada ya kuzozana na Rais Paul Kagame.

Familia yake ilisema kuwa lilikuwa ni jaribio la kumuua lakini serikali ya Rwanda imekanusha madai hayo.