Umoja wa Afrika kuongeza askari Somalia?

Uganda imeutaka Umoja wa Afrika kuongezea idadi ya askari wa vikosi vilivyotumwa kuiunga mkono serikali ya mpito nya Somalia. Sehemu ya vikosi vilivyoko sasa hivi ni kutoka Uganda vinavyosaidia kuhifadhi amani katika mji mkuu Mogadishu.

Wito huu ulitolewa na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kufuatia shambulio la bomu mjini Kampala lililowaua watu 74 wakati wakiangalia fainali ya Kombela Dunia.

Kundi la waasi la Al Shabab limedai kuwa lilifanya mashambulio hayo yaliyotokea wakati mmoja katika sehemu mbili tofauti.

Je kuna uwezekano wa Umoja wa Afrika kutuma askari zaidi huko Somalia na hatua hiyo itakuwa na athari yoyote katika usalama wa eneo hili la Afrika.

Image caption Wapiganaji wa Al-shabab wa Somalia

Kwa Al Shabab,shambulio hilo la siku ya jumapili ni ushindi bila kujali ni jinsi gani Umoja wa Afrika utapokea tukio hilo.

Kundi la Al Shabab lilidai kuwa lilifanya shambulio hilo kama kulipiza kisasi cha raia waliojeruhiwa na wengine kunyanyaswa na vikosi vya Uganda vilivyoko Somalia.

Vyama vya upinzani nchini Uganda vimeitaka serikali ivirejeshe vikosi hivyo nyumbani - hatua ambayo Al Shabab watashangilia kama ushindi mkubwa.

Halikadhalika, endapo Umoja wa Afrika utaitikia kilio cha Bw.Museveni kuongezea idadi ya vikosi badala ya kuondoa vilivyoko huko nalo linaonekana kusaidia hoja ya Al Shabab.

Mtaalamu wa shirika la kimataifa linalohusika na mgogoro wa Somalia, Rashid Abdi, ana amini kwamba kuweko huko Somalia kwa vikosi vya kigeni ni chachu ya Al Shabab kusajili wapiganaji wengine.

Rashid anasema kuwa Al Shabab imekuwa ikijitahidi kushawishi jamii ya Kiislamu nchini Kenya, Uganda na Ethiopia kuunda makundi yatakayolisaidia katika mapambano yake.

Kenya kwa upande mmoja, ina idadi kubwa ya Wakimbizi wa Kisomali - baadhi yao wakiwa muhimu katika kusambaza fedha na mapato kupitia biashara.

Mpaka dhaifu baina ya Kenya na Somalia nao pia upo wazi kwa waasi kupita bila upinzani, huku vyombo vya usalama wa dola vikiwa na mapungufu. Yote haya yanajiandaa kwa uwezekano wa mashambulizi mapya.

Milipuko ya Kampala sio tu ni ufunguo wa medani mpya katika vita dhidi ya Al Shabab bali medani nyingi tu.