Emile Heskey atundika viatu

Emile Heskey
Image caption Emile Heskey

Mshambuliaji wa timu ya soka ya England Emile Heskey ametangaza kustaafu kutoka soka ya kimataifa.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 alikuwa miongoni mwa kikosi kilichoongozwa na Fabio Capello huko Afrika ya kusini hadi hatua ya pili ya fainali za Kombe la Dunia.

Mara ya kwanza kwa Heskey kuichezea timu ya England ilikuwa mwaka 1999 dhidi ya Hungary na tangu hapo ameichezea mara 62 akifunga magoli saba.

Kwa kauli yake binafsi mchezaji huyo anasema, ''Nimefurahia kila nilipoichezea timu ya Taifa langu kwa fahari na furaha''

Nawashukuru viongozi wote wa timu hii walioniwezesha kushiriki pamoja na mashabiki walioniunga mkono katika kipindi chote nilipovaa jezi ya timu ya England.

Heskey alikuwa miongoni mwa timu ya England ya mwaka 2002 iliyoshiriki Kombe la Dunia halikadhalika kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Ulaya ya mwaka 2000 na 2004.

Aliweza kufunga bao kwenye mashindano ya mwaka 2002 dhidi ya Denmark lakini alishindwa kufunga bao lolote huko Afrika ya kusini England ilipopambana na Marekani na Algeria kabla ya mchuano dhidi ya Slovenia na kupoteza mechi ya Ujerumani.

Heskey alishiriki Kombe la Dunia mwaka huu huko Afrika ya kusini licha ya kuwa na msimu usioridhisha kwa klabu yake ya Aston Villa lakini kocha Capello alimuamini kufanya vyema akimuweka safu ya ushambuliaji pamoja na Wayne Rooney.

Mashabiki wengi na wachambuzi wa soka hawakukubaliana na uamuzi wa kocha kwa hoja kwamba licha ya umbo kubwa, Heskey ameshindwa mara nyingi kutikisa nyavu za upinzani.

Pamoja na kwamba alisaidia kwa mgongeo aliompitishia Steven Gerard katika sare ya 1 - 1 dhidi ya Marekani alishindwa kumalizia alipobaki na kipa wa Marekani mpira ukaishia miguuni mwa kipa.

Aliingia zikisalia dakika 19 za mchuano dhidi ya Ujerumani wakati Ujerumani ikiongoza bao 3 - 1.