Mahakama yaamuru Lubanga kuachiwa huru

Thomas Lubanga
Image caption Thomas Lubanga

Majaji katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu huko the Hague imemwamuru mshukiwa katika kesi ya kwanza-Thomas Lubanga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo-aachiliwe huru.

Hata hivyo, hatoachiwa huru kwa takriban siku tano, huku waendesha mashtaka wakifikiria iwapo wakate rufaa au la.

Kesi hiyo iliahirishwa wiki iliyopita baada ya majaji kugundua kuwa kuna taratibu zilizokuwa hazijafuatwa.

Bw Lubanga amekana mashtaka ya kuwatumia watoto kama wanajeshi.

Ofisi ya mwendesha mashitaka- Luis Moreno Ocampo- imeonekana kutoweza kumpata shahidi.

Jaji Adrian Fulford amesema Bw Lubanga anatakiwa 'kuachiwa bila masharti yeyote' akisema kuwekwa kwake kizuizini "haikuwa kwa haki" baada ya kesi hiyo kuahirishwa.

Katika uamuzi wao, majaji wamesema: " Mshtakiwa hawezi kushikiliwa kwa misingi ya kushuku, ambapo katika hatua nyingine hapo baadae kesi hiyo inaweza kuanza upya."

Hata hivyo, upande wa mashtaka una siku tano kuomba rufaa, iwapo itakubalika, Bw Lubanga atabaki kizuizini mpaka rufaa hiyo isikilizwe.

Inaaminika kuwa upnade wa mashtaka utakata rufaa.

Kesi ya Bw Lubanga, iliyoanza mwaka 2009 baada ya kuchelewa kwa miezi saba juu ya mgogoro wa kutumia ushahidi wa siri, umejikuta katika changamoto nyingi za kisheria.

Shahidi wa kwanza alikanusha maelezo yake ambapo awali alisema aliajiriwa na wapiganaji wa Bw Lubanga akirejea nyumbani wakati akitoka shule.

Tatizo moja linaloikabili mahakama hiyo ni kwamba Bunia- mji mkuu wa Ituri ambapo Bw Lubanga alikuwa kiongozi wa waasi- bado inachukuliwa kama eneo la vita.

Hii inamaanisha usalama wa mashahidi hauna uhakika.

Bw Lubanga alikiongoza chama cha Union of Congolese Patriots (UPC), wanamgambo wa kabila ya Hema, moja miongoni mwa makundi sita yaliyopigana kudhibiti eneo lenye utajiri wa dhahabu kwenye mji wa Ituri kuanzia mwaka 1999 hadi 2003.

Mapigano hayo yaligeuka na kuwa vita vya kikabila ambapo takriban watu 50,000 waliuawa na maelfu walibaki bila makazi.