Filamu ya bin Laden marufuku Pakistan

Image caption Ramani ya Pakistan

Bodi inayosimamia filamu nchini Pakistan imepiga marufuku mchezo wa kuigiza unaomhusu Osama Bin Laden kuonyeshwa nchini humo.

Mchezo huo uliopewa jina la Tere Bin Laden, unasimulia visa vya mtu anayefanana na mtu anayetakikana kuliko wote duniani.

Kampuni kuu inayosambaza filamu hiyo imeiambia BBC kuwa imekata rufaa kupinga uamuzi huo.

Bw Nadeem Mandviwala amesema kwa sasa amewasilisha hoja yake kwenye wizara ya utamaduni.

Kabla ya hapo, bodi inayosimamia filamu ilitaja sababu za kuizuia filamu hiyo isonyeshwe.

Sababu kuu ilikuwa kumuonyesha Osama Bin Laden kama kichekesho. Sababu nyingine ni matumizi ya lugha isiyostahili, pamoja na kile kilichotajwa kama kudhalilisha vyombo vya sheria nchini humo katika filamu hiyo.

Ingawa hatua hii haikutarajiwa hakuna la kushangaza kutokana na kwamba serikali ya nchi hiyo haipendi kugusia wala kujihusisha na suala la Osama Bin Laden.

Ingawa hajulikani alipo, maofisa wa Marekani wana imani kuwa bado yumo mafichoni nchini Pakistan.

Pamoja na hayo yote, Bw Mandviwala amesema ana imani kuwa kikwazo hicho kitaondolewa.

Wizara ya utamaduni itatangaza uamuzi wake.