Wakili mtetezi wa ICTR auawa Tanzania

Image caption Yussuf Munyakazi

Wakili mwandamizi wa utetezi nchini Tanzania wa mahakama inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa inayoshughulikia kesi za washukiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda amepigwa risasi na kufa nje ya nyumba yake mjini Dar es Salaam.

Profesa Jwani Mwaikusa, ambaye pia alikuwa mkufunzi katika chuo kikuu cha Dar es Salaam, aliuawa wakati akitaka kuingia nyumbani kwake nje kidogo ya mji huo.

Polisi wanasema mpwa wake pamoja na jirani yake waliuawa pia.

Imearifiwa kuwa wahalifu hao walilipekua gari la marehemu na kuondoka na mkoba wake wa kazi pamoja na hati kadhaa.

Bw Mwaikusa alikuwa wakili mtetezi wa mfanyabiashara wa Rwanda Yussuf Munyakazi anayekabiliwa na tuhuma za kuhusika katika mauaji ya kimbari kwenye mahakama ya kimataifa mjini Arusha.

Wakati akimtetea, alifanikiwa kuzuia Munyakazi asirejeshwe nchini Rwanda, kwa hoja kuwa asingeweza kutendewa haki na mahakama za huko.

Gazeti la Citizen nchini Tanzania limesema kumekuwepo na ongezeko la matukio ya uhalifu mjini Dar es Salaam katika siku za hivi karibuni.

Watu watano wameuawa kwa risasi na wahalifu wenye silaha katika kipindi cha miezi mwili iliyopita.