BP yafanikiwa kuziba kisima kinachovuja

Image caption Sehemu ya kisima kilichozibwa maelfu ya mita chini ya bahari.

Kampuni ya mafuta ya BP inasubiri matokeo ya majaribio yaliyofanywa kwenye kisima cha mafuta kilichokuwa kinavuja katika Ghuba ya Mexico, siku moja baada ya kufanikiwa kukiziba kwa mara ya kwanza tangu mwezi Aprili.

Kampuni hiyo inatathmini kuona mgandamizo kiasi gani wa mafuta unasukuma kisima hicho, wakati valvu zinapofungwa.

Rais Barack Obama wa Marekani ameelezea hatua hiyo kuwa ni "dalili njema", na hisa za BP zilipanda thamani katika masoko ya London kama zilivyopanda New York.

Mafuta yalikuwa yakivuja katika kisima hicho tangu kulipotekea mlipuko tarehe 20 mwezi Aprili.

Athari

Wafanyakazi 11 waliuawa kwenye mlipuko katika kisima cha Deepwater Horizon, na mafuta yaliyovuja yalisababisha wasi wasi wa uharibifu mkubwa wa mazingira.

Awali BP ilijaribu mbinu kadhaa kujaribu kuzuia uvujaji huo, lakini uzibaji huo mpya ni wa kwanza kufanikiwa kuzuia kabisa mafuta.

Afisa mwandamizi wa BP, Kent Wells, alitangaza mafanikio siku ya Alhamisi, akisema "nimefurahishwa" na mafanikio hayo.

Kampuni hiyo itakagua kwa karibu uimara wa kisima kwa kufanya vipimo vya kina mpaka siku ya Jumamosi.