Wachezaji kamari haramu wanaswa Asia

Nembo ya polisi wa Interpol
Image caption Nembo ya polisi wa Interpol

Zaidi ya watu 5,000 wamekamatwa na zaidi ya dola milioni 10 kunaswa na polisi wa kimataifa Interpol, katika msako uliofanyika Asia, na kulenga uchezaji kamari haramu wakati wa Kombe la Dunia.

Waliokamatwa wanaripotiwa kuwa na uhusiano wa karibu na magenge ya uhalifu. Msako huo uliodumu kwa muda wa mwezi mmoja ulijulikana kama SOGA3 na ulianza punde tu baada ya kombe la dunia kuanza.

Msako huo uliendeshwa na makao makuu ya Interpol nchini Ufaransa, kwa ushirikiano na maafisa wa China, Hong Kong, Macau, Malaysia, Singapore na Thailand.

Maafisa wa hao walinasa mamilioni ya dola, magari, kadi za benki, komputa na simu za mkononi.

Polisi wanasema kuna ushahidi wa kuonyesha washukiwa hao wana uhusiano na magenge ya uhalifu, yanayohusishwa na uhamishaji haramu wa fedha na ukahaba.

Mkuu wa polisi wa Interpol mjini Lyon, amesema ushirikiano kati ya maafisa wake na maafisa wa nchi nyingine, ulifanikisha msako huo ambao ameutaja kuwa wa aina yake.

Polisi walivamia takriban maeneo 800 ya uchezaji kamari haramu wakati wa Kombe la Dunia.