Mwanamama avaa gauni la spinachi Kenya

Image caption Michelle Odhiambo akiwa katika vazi lake la mboga aina ya spinach.

Mwanaharakati aliyevaa gauni lililotengenezwa kwa spinachi amefanya maonyesho huko Nairobi, Kenya katika kampeni ya kushawishi Wakenya kuacha kula nyama.

Michelle Odhiambo, anayejulikana kama ''The Lettuce Lady" ni kutoka shirika linalotetea haki za wanyama. Amesema kampeni yake ina malengo mawili.

Kwanza nguo yake inahimiza watu kula mboga za majani na pili kuhimiza watu kutokula nyama ya kuchoma maarufu sana nchini Kenya kama ''nyama choma''.

Bi Odhiambo, ambaye aliacha kula nyama miaka minane iliyopita amesema chakula ambacho hutumiwa kulisha wanyama wanaochinjwa kinaweza kutumiwa kulisha watu wengi.

Huku akibeba bango lililoandikwa "Let Vegetarianism Grow On You" aliambia watu waliojitokeza kumuona kuwa pia ana wasiwasi kuhusu jinsi wakulima hushugulikia mifugo.

''Mifugo wanafungiwa katika maeneo madogo sana, wanawahasi, wanawachinja na haya yote wanafanya bila kuwapa dawa za kudhibiti uchungu. Hiyo ni haki kweli?''

Bi Odhiambo pia ametoa wito kwa migahawa kubadilisha mapishi na kuwafikiria zaidi watu wasiopendelea kula nyama.

Mwandishi wa BBC mjini Nairobi anasema kupika chakula bila nyama, hasa katika maeneo ya mijini ni jambo linalohusishwa na umaskini nchini Kenya.

''Sasa tutakula nini tusipokula nyama?'', aliuliza Mohamed Asman, kutoka Kaskazini Mashariki mwa Kenya ambako kuna jamii ya wafugaji na nyama ndiyo chakula chao cha kila siku.