Waziri Mkuu Uhispania asusa kumwona Kagame

Rais Kagame wa Rwanda
Image caption Rais Kagame wa Rwanda

Waziri Mkuu wa Uhispania Jose Luis Rodriguez Zapatero amesusia kukutana na Rais wa Rwanda, kufuatia ombi kutoka kwa vyama vya kisiasa kikiwemo chama chake.

Mkutano huo ulikuwa wa kwanza kati ya mfululizo wa mikutano iliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa yenye kutathmini mafanikio ya malengo ya maendeleo duniani ya millenium, ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya ufukara na vifo vya watoto wadogo.

Uamuzi huu wa Bw Zapatero ulikuwa ni wa dakika za mwisho. Yeye mwenyewe hakuzungumzia suala hillo, ila naibu wake amesema waziri mkuu alipokea maombi kutoka kwa vyama kadhaa vya kisiasa vya Uhispania ili asikutane na Rais wa Rwanda.

Naibu waziri mkuu alisema Bw Zapatero aliyachukulia maombi hayo kwa uzito na kukubaliana nayo.

Kwa hivyo mkutano huo ambao ulifadhiliwa na Umoja wa Mataifa na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, ulihamishiwa kwenye hoteli, na Uhispania badala yake ikawakilishwa na waziri wake wa mambo ya kigeni.

Mgogoro huo wa kidiplomasia unahusiana na mashtaka dhidi ya Rais wa Rwanda yaliyoanzishwa na jaji mwandamizi wa Uhispania miaka miwili iliyopita.

Jaji huyo alitoa hati ya kukamatwa kwa wanajeshi 40 wa Rwanda, akiwashtumu kutekeleza mauaji makubwa ya kulipizia kisasi dhidi ya jamii wa Kihutu mwaka wa 1994, baada ya mauaji ya kimbari ya maelfu ya jamii ya Kitutsi.

Wanajeshi hao wakati huo walikuwa chini ya utawala wa Rais Kagame - lakini Kagame ni rais wa nchi na ana kinga ya kumlinda dhidi ya mashtaka.

Mwezi uliopita, kiongozi wa Rwanda aliteuliwa kuwa mwenyekiti mwenza na Bw Zapatero wa kundi lenye majukumu ya kuhakikisha utekelezaji wa malengo ya millenia.

Ban Ki Moon alimchagua Kagame kutokana na mchango wake wa mafanikio ya Rwanda katika kupunguza vifo vya watoto.

Bw Ban alisita kuzungumzia akiwa mjini Madrid madai ya mahakama hiyo ya Uhispania.

Siku ya Ijumaa, Waziri Mkuu Zapatero aliwapokea wageni wote wa mkutano huo ofisini kwake -isipokuwa Rais Kagame wa Rwanda.