Mubarak kukutana na viongozi wa mashariki ya kati

Rais Hosni Mubarak
Image caption Rais Hosni Mubarak

Rais wa Misri Hosni Mubarak atakuwa mwenyeji wa mikutano mbali mbali mjini Cairo, ambayo inalenga kufufua mazungumzo ya amani katika Mashariki ya Kati.

Mubarak atakutana na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, Rais wa Palestina Mahmoud Abbas, na mjumbe maalum wa Marekani katika Mashariki ya Kati, George Mitchell.

Kwa kuchukua hatua kama hiyo Misri inaanzisha tena nafasi yake kitamaduni ya kuwa mpatanishi, ikiwa ni sehemu ya kujaribu kufufua mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Israel na Wapalestina.

Rais Obama ana nia ya kuona mpango wa amani wa Mashariki ya Kati unapiga hatua.

Waziri Mkuu wa Israel, Bw Netanyahu anaonekana kutoa ushirikiano katika suala hili.

Lakini Wapalestina wanahofia kuwa Waisraeli wanaongea tu ili kuifurahisha Marekani, bila kuchukua hatua thabiti za kuweza kufikiwa kwa maridhiano.

Hata hivyo, kuna dalili kuwa Rais Mahmoud Abbas atakuwa tayari kurejea katika mazungumzo ya moja kwa moja.

Ziara hii nchini Misri itakuwa njia nzuri kwake kupata uungwaji mkono wa nchi za Kiarabu kwa hatua kama hiyo ya kufanya mazungumzo ya ana kwa ana Israel.

Rais Mubarak kuwa na shughuli nyingi za kidiplomasia kwa siku moja pia ni jambo zuri linaloonyesha kuwa baado ni mzima ,kufuatia uvumi kuwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 hana hali nzuri ya kiafya.