Tishio la mafuta kuvuja Ghuba ya Mexico

Kampuni ya mafuta ya BP imekubaliwa kutoondoa kifuniko cha kisima chake kinachovuja mafuta katika Ghuba ya Mexico japo kwa muda.

Afisa wa Marekani anayehusika katika shughuli ya kusafisha mafuta yaliyovuja baharini, amesema kifuniko hicho kitaendelea kuwepo kwa muda wa saa 24.

Tangu kampuni ya BP ilipoweka kifuniko kipya, imekuwa ikifanya majaribio ili kuthibitisha kama mafuta yameacha kuvuja.

Afisa huyo ameitaka kampuni ya BP kuweka mpango wa kuondoa kifuniko iwapo mafuta yanaendelea kuvuja.

Hata hivyo, kampuni hiyo inasema itachukua muda wa siku tatu kuanza kushugulikia tatizo hilo.

Iwapo kifuniko hicho kitatolewa, huenda melfu ya mapipa ya mafuta yakavuja kama ilivyokuwa hapo awali.

Uvujaji wa mafuta katika Ghuba ya Mexico umetajwa kuwa janga baya zaidi la uharibifu wa mazingira kusababishwa na binadamu kuwahi kutokea nchini Marekani.

Hali hiyo imeathiri eneo kubwa la bahari ya Ghuba ya Mexico, na pia watalii wamesusia kuzuru bahari hiyo na hata shughuli za uvuvi kusitishwa.

Kampuni ya BP imekadiria kuwa fedha za kushugulikia janga hilo zitakuwa zaidi ya dola bilioni nne.

Tayari kampuni hiyo imetumia zaidi ya dola milioni 200 kulipa fidia.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, atakutana na Rais Obama wa Marekani mjini Washington siku ya Jumanne, ambapo swala la BP linatarajiwa kuwa katika ajenda ya mkutano huo.