Kasisi wa Kenya ashtakiwa kuwa na 'bomu'

Kasisi wa Kenya amekana mashtaka mawili ya madai ya njama za kutega bomu katika maandamano ya kuipinga katiba mpya.

John Kamau Mbugua na wanaume wengine wawili walikamatwa siku ya Jumamosi, wakidaiwa kuwa na mbolea na milipuko.

Polisi wamesema alikuwa na mpango wa kwenda Mombasa, ambapo makanisa yalikuwa yamesaidia kuandaa maandamano ya kuipinga katiba hiyo.

Mwezi uliopita, shambulio la guruneti katika maandamano ya kanisa hilohilo yalisababisha vifo vya watu sita.

Siku chache kabla ya kupiga kura ya maoni Agosti 4, baadhi wanahofia kuibuka kwa ghasia za kisiasa.

Takriban watu 1,300 waliuawa na 300,000 walilazimika kuhama makazi yao baada ya mgogoro wa uchaguzi wa Desemba 2007.

Huko mahakamani, Bw Mbugua alisema yeye ni kasisi wa kanisa la Victory, ijapokuwa maafisa wa kanisa wanasema alitengwa na kanisa miaka mitatu iliyopita.

Pia ni afisa wa chama cha Rais Mwai Kibaki cha National Unity (PNU).

Rais Kibaki pamoja na Waziri mkuu Raila Odinga wanafanya kampeni kuiunga mkono rasimu mpya ya katiba hiyo.

Baadhi ya makanisa yanaipinga katiba hiyo mpya kwasababu inatambua mahakama za kiislamu.