Mabomu yarushwa shule ya Quran Somalia

Watoto 10 wamejeruhiwa baada ya bomu kulipuka katika shule moja inayofundisha Quran mjini Mogadishu.

Tukio hilo limetokea wakati wa mapigano mapya kati ya vikosi vya Somalia na wapiganaji wa al-shabab.

Image caption Mtoto mdogo akiongoza kundi la al-Shabab

Mapigano yaliyoendeshwa na vikundi vinavyohusishwa na Al-qaeda yalianza Jumapili yakilenga ofisi za serikali na Umoja wa Afrika katika wilaya za Bondhere na Shibi.

Maafisa wa uokoaji wamesema, karibu watu 10 wameuawa na wengine 40 kujeruhiwa.

Serikali ya mpito inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imekuwa ikihangaika kuwadhibiti waasi ambao wako eneo la kusini mwa Somalia.

Shule iliyopigwa kwa bomu iko katika wilaya ya Hamarweyne, moja ya maeneo machache ambayo yanashikiliwa na serikali mjini Mogadishu.

'Bomu liliangukia jengo la shule wakati watoto wakijiandaa kwenda nyumbani,' Mo'allin Ali Mohamud, mwalimu katika shule hiyo aliiambia BBC, 'Wanafunzi wangu 10 walijeruhiwa vibaya'

Mkazi mmoja Aden Haji Ilmi alisema, 'Wakati wapiganaji walipokuwa wakijaribu kuwasukuma askari wa serikali kaskazini kuelekea kwenye kituo cha Umoja wa Afrika, mabomu mazito yalirushwa eneo jirani yanayodhibitiwa na waasi."

Dahabo Nurre, mama wa watoto sita aliiambia BBC: "Tuliendelea kujificha chini ya jengo kijijini kwetu kwa saa kadhaa kwa sababu mabomu yalitupwa ovyo na mengine yaliangukia kwenye makazi ya watu."

Mapigano yalikuwa makali tangu al-Shabab wapige mabomu nchini Uganda wakati wa fainali za Kombe la Dunia Julai 11.

Mashambulio hayo yaliilenga Uganda kwa sababu ina majeshi yake nchini Somalia chini ya mpango wa kulinda amani wa AU amabyo yanaisaidia serikali.