Sudan kujadili mustakabali wa eneo la kusini

Salva Kiir rais wa Sudan Kusini

Kikao cha leo ni muhimu sana katika kuangazia mstakhabali wa nchi kubwa zaidi barani Afrika. Viongozi wa Kuu kutoka Kaskazini na Kusini mwa Sudan wanakutana pamoja miezi sita kabla ya kura muhimu zaidi ya maoni itakayoamua uhuru wa eneo la Kusini.

Mazungumzo ya leo yametajwa kuwa muhimu na kwa siku mbili kamati ya wataalamu itakuwa na jukumu la kutathmini pande tofauti. Kwanza hali itakuaje, ikiwa wengi wataunga mkono kusini kujitenga kama ilivyo imani ya raia wengi wa eneo hilo.

Kuna uwezekano wa kuzuka mgawanyiko mkubwa miongoni mwa makundi tofauti hususan kuhusu masuala ya Uraia, Maeneo ya mipaka, deni la nje lililotolewa kwa Sudan, na jinsi ya kugawanya raslimali ya Mafuta inayopatikana kwa wingi kusini japo mafuta yenyewe yanaelekezwa kwa mabomba yaliyo kaskazini.

Kura ya Maoni iliafikiwa chini ya mkataba wa amani wa mwaka 2005 ambao ulimaliza vita vya miongo miwili.

Muungano wa Afrika Pamoja na jamii ya kimataifa zimeelezea wasi wasi kuwamba muda unayoyoma huku masuala tata yanayohusiana na kura ya maoni yakiwa bado kuangaziwa hali inayotishia kurejelewa vita ikiwa hayatatatuliwa.

Japo shughuli ya upatanishi ingali kuanza, mazungumzo ya leo yameonekana kuleta matumaini kwa wengi. Hata hivyo changamoto kubwa itakuwa kuafikia maazimio yatakayokubaliwa na pande zote.

Kando na kikao cha viongozi, kunayo kamati maalum ambayo imeundwa kuangazia kura ya maoni ya eneo linalozozaniwa la Abyei.

Eneo hili lenye utajiri wa mafuta litapiga kura sambamba na jirani zao wa Kusini kuamua ikiwa watasalia chini ya utawala wa kaskazini au kuwa chini ya serikali huru ya Kusini.