Picha za 'walipuaji mabomu' zatolewa

Image caption Picha za washukiwa wa mabomu Uganda

Picha za watu wawili ambao polisi wanaamini walihusika na milipuko ya mabomu nchini Uganda wiki moja iliyopita zimetolewa.

Shirika la kimataifa la upelelezi la Interpol limeanza kusambaza picha zinazoonyesha namna wanavyoona sura zao zinavyoonekana.

Polisi wamekuta vichwa viwili visivyotambulika baada ya milipuko ya mabomu hayo ya Kampala yaliyosababisha vifo vya takriban watu 73, na wanaamini ndio waliohusika na mashambulio ya kujitoa mhanga.

Takriban watu 73 waliuawa katika klabu ya raga na mgahawa siku ya fainali ya Kombe la Dunia.

Kundi la kisomali la al-Shabab limesema limehusika na milipuko hiyo.

Majeshi ya Uganda ni sehemu ya jeshi la Umoja wa Afrika linalounga mkono serikali ya mpito ya Somalia.

Miili hiyo miwili inayoonekana kuathirika na milipuko hiyo imebaki bila kuuliziwa na mtu na wala kutambuliwa, ambapo polisi wamesema imesababisha waamini kuwa shambulio hilo limefanywa na watu waliojitoa mhanga.

Mkuu wa polisi Kale Kayihura aesema kwenye mkutano wa waandishi wa habari kwenye mji mkuu wa Uganda, " Mashambulio haya yamefanywa na watu waliojitoa mhanga. Ushahidi unalionyesha hili wazi kabisa."

"Vichwa viwili mpaka sasa havijauliziwa na yeyote, na wala havijatambuliwa. Haiwezekani matukio haya mawili yakatokea kwa pamoja."

Bw Kayihura amesema pia utengenezaji wa sura za washukiwa wa mabomu hao unapendekeza mmoja ni mwenye asili ya Kisomali na mwengine ni mwafrika mweusi ambaye asili yake haijajulikana.

Bw Kayihura alisema "Kwa kutoa picha hizo hadharani, tunaamini kuna mtu, pahala popote ambaye ataweza kumtambua mmoja au wote wawili."

Serikali ya Uganda imewakamata zaidi ya watu 20 huku wakiendelea na uchunguzi wa mashambulio hayo.

Takriban watu 60 waliouawa ni wa kutoka Uganda. Wengine waliofariki dunia ni kutoka mataifa ya Ethiopia, Eritrea, India na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na mmoja kutoka Ireland na Marekani.

Wengine wengi bado wanatibiwa hospitalini kutokana na majeraha.