Mwili wa mwanasiasa wa Rwanda kuchunguzwa

Mauaji Rwanda
Image caption Mauaji Rwanda

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, linataka mwili wa mwanasiasa wa Rwanda aliyeuawa wiki iliyopita, ufanyiwe upasuaji na uchunguzi huru ili kubaini jinsi mauaji hayo yalivyotokea.

Polisi wanasema wanaamini kuwa mauaji ya mwanasiasa huyo Andre Kagwa Rwisereka,yalikuwa ya kulipiza kisasi kutokana na mzozo wa kibiashara.

Mwili wake ulikutwa umetupwa karibu na nyumbani kwake Kusini mwa Rwanda .

Polisi wamemkamata mshukiwa mmoja, anayedaiwa kuwa mshirika wake wa kibiashara. Lakini shirika la Human Rights Watch linasema mauaji hayo yalifanywa kwa misingi ya kisiasa.

Bw Rwisereka alikuwa amewaambia washirika wake wa karibu kuwa alikuwa akipewa vitisho kwasababu ya kupinga chama tawala cha RPF.

Shirika la Human Rights Watch, linasema uchunguzi huru utakaohusisha maafisa wa kigeni unapaswa kufanywa ili kubaini kilichotokea.

Mauaji ya Rwisereka yametokea baada ya mashambulio mengine kadhaa kufanywa dhidi ya wapinzani wa Rais Paul Kagame.

Image caption Jenerali Nyamwasa aliyepigwa risasi Afrika Kusini

Mwezi uliopita aliyekuwa mkuu wa jeshi la Rwanda Jenerali Kayumba Nyamwasa, alipigwa risasi nchini Afrika Kusini na kujeruhiwa. Jenerali huyo anadai kuwa shambulio hilo lilikuwa jaribio la kumuua.

Muda mfupi baada ya shambulio hilo, mwandishi wa habari Jean Leonard Rugambage, akapigwa risasi na kuuawa mjini Kigali.

Serikali ya Rwanda imekanusha vikali kuhusika na mashambulio hayo, ambayo yamesababisha wasiwasi na uoga miongoni mwa wapinzani wa serikali. Baadhi ya wanasiasa wanasema wametishwa na kunyimwa haki ya kushiriki katika uchaguzi ujao.