Slaa ataka urais Tanzania kupitia CHADEMA

Image caption Dr Wilbroad Slaa, mgombea wa CHADEMA uchaguzi wa Rais Tanzania.

Chama cha upinzani huko Tanzania, cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, kimemteua Dr Wilbroad Slaa kuwa mgombea wake katika kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka huu.

Tangazo la kuteuliwa kwa Dr Slaa lilitolewa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, jijini Dar Es Salaam siku ya Jumatano.

Bw Mbowe alisema kwenye makao makuu ya CHADEMA kuwa kwa kauli moja kamati kuu ya chama chake imekubaliana kwa kauli moja kumuomba Dr Slaa kugombea nafasi ya urais, na kwamba naye amekubali.

Mbowe alipingana na mtizamo kuwa hatua ya kumteua Dr Slaa kwa kazi hiyo itapunguza makali ya upinzani bungeni, baada ya kuwa akigombea kiti cha rais moja kwa moja hataweza kugombea tena ubunge wa jimbo la Karatu ambao ndiyo umempa umaarufu mkubwa.

Kiongozi huyo wa CHADEMA alisema hawana wasiwasi wa kupoteza jimbo la Karatu kwa maelezo kuwa hakuna chama chenye nguvu ya kulitwaa jimbo ambalo halmashauri yake ya wilaya imekuwa ikiongozwa na CHADEMA kwa takriban miaka 10.