Hillary Clinton ziarani Korea Kusini

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton
Image caption Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Hilary Clinton, pamoja na mwenziye wa Ulinzi Robert Gates, wako nchini Korea ya Kusini kwa ajili ya mfululizo wa mazowezi ya jeshi la wanamaji baina ya nchi hizo mbili.

Mazoezi hayo yanaanza mwishoni mwa juma hili, huku mawasiliano ya ngazi ya kibalozi yakikusudia kuifariji Korea ya kusini kufuatia kupoteza manuwari yake mnamo mwezi machi mwaka huu.

Kuzama kwa manowari ya Korea ya Kusini iliyokuwa ikijulikana kama Corvette mapema mwezi machi mwaka huu kulizua upya mvutano baina ya Korea ya kaskazini na Kusini.

Wanamaji arobaini na sita walipoteza maisha yao kwenye tukio hilo na Korea ya Kaskazini iliyolaumiwa imesisitiza kuwa haikuhusika.

Halikadhalika hali ya sintofahamu inayozidi kuongezeka ndani ya Korea ya Kaskazini imesababishwa na kile wadadisi wengi wanachosema ni ubishi juu ya nani atakayerithi mamlaka kutokana na hali mbovu ya afya ya kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong il.

Hofu kubwa iliyopo ni kwamba serikali ya Korea ya Kaskazini isiyotabirika, inaweza kutumia mazowezi haya kama kisingizio cha hatua yoyote ya kijeshi bila kutarajiwa.

Hiyo ni sababu moja inayowatisha Wachina kuhusu mazoezi haya. Msemaji wa wizara ya kigeni ya Uchina, amezitaka pande zinazohusika zijitahidi kuwa tulivu na wasichochee kwa vyovyote vile jambo litakalozusha mtafaruku katika kanda nzima.

Huu ni ujumbe uliolenga siyo tu viongozi wa Korea ya Kaskazini au Kusini bali pia Marekani. Vilevile Uchina haijafurahia mazoezi haya kwa sababu zake pia. Kwa mujibu wa ratiba, mazoezi ya baadaye yatafanyika katika bahari ya Yellow iliyo katikati ya rasi ya Korea na Uchina.

Kwa Uchina maji haya ni maeneo muhimu yanayoelekea mipaka yake.