Mwili wa Ceausescu wa Romania wafukuliwa

Image caption Nicolae Ceausescu

Wataalamu nchini Romania wamefukua kinachoaminika kuwa mabaki ya aliyekuwa kiongozi wa Romania, Nicolae Nicolae Ceausescu na mke wake kwa ajili ya uchunguzi wa kuthibitisha kama kweli walizikwa mahali hapo.

Hii ni kufuatia ombi la familia yake iliyohoji kama wazazi wao kweli walizikwa katika makaburi ya Ghencea mjini Bucharest.

Nicolae Ceausescu alitawala Romania kuanzia mwaka 1965 hadi alipopinduliwa katika mapinduzi ya mwaka 1989.

Yeye na mke wake walikamatwa wakati wakijaribu kukimbia nchi na kunyongwa pamoja.

Inaaminika maiti zao zilizikwa kwa haraka haraka katika kaburi ambalo halikuwekwa majina kwenye makaburi ya kijeshi.

Suala kubwa ambalo limekuwa likiwatatiza wasomi na raia wa Romania ni mahali walipozikwa akina Ceacescu.

Sasa mtoto pekee aliyenusurika mauaji yaliyofuatia mapinduzi, Valentin pamoja na shemeji yake wamesema kuwa wanataka kutambua maiti za wazazi wao hao.

Mapema Jumatano wataalamu wa kitabibu pamoja na wasimamizi wa makaburi walionekana wakichukua mifano kutoka maiti kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa asidi nasaba DNA.

Mkwe wa Ceacescu, Mircea Oprean alinukuliwa akisema anadhani mabaki hayo ni ya wakwe zake ingawa alitaka kusubiri matokeo ya uchunguzi wa asidi nasaba DNA.

Aliongezea kuwa alihisi mwili wa baba mkwe wake ulihifadhiwa vizuri, akitambua koti lake jeusi la majira ya baridi.

Gelu Voican-Voiculesc, akiwa ofisa aliyeongoza serikali baada ya kumuangusha Ceausescu, alisimamia mazishi mnamo mwaka 1989 na kusema uchunguzi huo utathibitisha alichosema kuwa daima amehimiza kuwa walizikwa hapo.

Uchunguzi wa asidi nasaba unaweza kuchukua hadi miezi sita, kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari nchini Romania.